Bosi auawa, atumbukizwa kwenye shimo la choo chake

Rombo. Mkazi wa Kijiji cha Ubetu wilayani hapa, Rogasian Onesfory (60) anadaiwa kuuawa kwa kukatwa na panga sehemu za kichwani na mfanyakazi wake wa ndani wa kiume kisha kutumbukizwa kwenye shimo la choo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa alisema jana kuwa tukio hilo lilitokea Juni 25, baada ya mzee huyo kutoka sokoni kuuza nguruwe wake kwa Sh800,000.

Mwili wa mzee huyo uligundulika siku mbili baadaye ukiwa ndani ya shimo la choo.
Kamanda Maigwa alisema: “Ni kweli hili tukio lipo na zipo taarifa kwamba baada ya huyu baba kuuza nguruwe wake alipata fedha, ndipo mfanyakazi wake akachukua jukumu la kumuua na kukimbia, bahati nzuri tumemfahamu aliyefanya hilo tukio, tutamkamata tu.”

Kamanda Maigwa alisema ndugu wa mzee huyo, Erasmi Onesfory ambaye ni balozi wa nyumba kumi, alisema tangu Juni 25 ndugu walijaribu kumtafuta kwa njia ya simu na hakupatikana kwa siku kadhaa.

Alisema baadhi ya ndugu waliokuwa jirani walimtafuta kwa kushirikiana na majirani na walipofika nyumbani anakoishi mzee huyo hawakumkuta, lakini walimkuta mfanyakazi wake.

Alisema waliendelea kumtafuta mzee huyo bila mafanikio, ndipo kijana huyo aliyekuwa anaishi naye aliwaeleza huenda mzee baada ya kuuza nguruwe wake alikwenda Dodoma kwa familia yake.

Kamanda Maigwa alisema licha ya majibu hayo, ndugu zake na familia waliopo Dodoma walikuwa wakimtafuta kwa njia ya simu bila mafanikio.
Alisema baadaye walifanya jitihada za kuitana majirani pamoja na ndugu wengine hadi nyumbani kwa mzee huyo na kukuta milango imefungwa na kijana hayupo nyumbani.

Kamanda alisema Juni 27 jioni walipofika tena nyumbani kwa mzee huyo kulikuwa na sehemu kumemwagwa maji kama kuna kitu kimefanyika, ndipo waligundua kuna matone ya damu.

Alisema walifuatilia matone hayo yanapoelekea na walipofika eneo la choo walichungulia ndani, ndipo walipoona mwili wa ndugu yao ukiwa ndani ya choo.

“Huyu ndugu yetu alitoweka tangu Juni 25, mwaka huu, tulifanya jitihada za kumtafuta hatukumpata, lakini tulipomuuliza kijana aliyekuwa akiishi naye hapo nyumbani ambaye ni mfanyakazi alituambia alienda kuuza nguruwe na hajarudi; alituambia huenda baada ya kuuza nguruwe wake ameenda Dodoma kwenye familia yake,” alisema Kamanda Maigwa.

“Tuliendelea kumtafuta bila mafanikio tangu siku ya tukio lakini jana jioni (juzi) tuligundua ndugu yetu ameuawa na kutumbukizwa kwenye choo cha hapa nyumbani kwake na hii inaonyesha kabisa ni mfanyakazi wake wa nyumbani aliyemwajiri ndio kamuua, baada ya kufanya mauaji hayo alikimbia.

Kibaya zaidi hatujui huyu mfanyakazi alimpata wapi, maana mwezi haujaisha tangu aje hapa nyumbani kwa ndugu yangu,” alisema.